Thursday, August 2, 2012

MAANA YA NAMBA 666


comments
Maandiko yanasema: ... siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo baba zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. (2 Petro 3:3-4).

Mtume Petro anatuambia hapa kwamba, watu watasema, “Kila siku mnasema, Yesu anakuja; Yesu anakuja. Yuko wapi? Mbona miaka inaenda tu. Msituzingue bwana!”
Je, hayo si ndiyo tunayoyasikia kila uchao? Mimi nimeshayasikia mara kadhaa. Naamini nawe pia umesikia dhihaka kama hizo.

Lakini maandiko yanasema kwamba: Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote waifikilie toba. (2 Petro 3:9).

Mungu anataka watu wote wamwamini Yesu na kupokea wokovu wa bure ambao Yeye aliulipia gharama kubwa ya uhai wake. Lakini nikwambie jambo: siku atakapotokea, hata kama kwa mtazamo wa kibinadamu ataonekana anachelewa, muda wote wa nyuma hautamfaidia kitu kamwe mtu ambaye hakumwamini Yeye ajaye! Cha msingi ni je, wakati huo atakukuta katika mkao gani kiimani?utakavyokuwa wakati huo ndicho kitakachoamua hatima yako ya milele!

Katika nyakati hizi tulizo nazo, dunia inajiandaa kuingia wakati wowote kwenye kipindi ufalme wa kuzimu wa moja kwa moja. Shetani atakuwa anatawala dunia moja kwa moja.

Kwa sasa, japo shetani yupo na anatenda kazi, lakini ni kwa kiwango cha chini. Maandiko yanasema: Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. (2 Wathesalonike 2:6-12).

Sasa huyu asi anapitia wapi? Biblia inasema kwamba: Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. (1 Timotheo 6:10).
Fedha ni kitu kizuri na muhimu sana katika maisha yetu. 

Lakini hapo pia ndipo penye nguvu na mlango wa kuzimu. Fedha au biashara au kwa túseme uchumi, vitahusika sana katika nyakati za mwisho za utawala wa shetani hapa duniani. Huu ni utawala ambao kimsingi maandalizi yake ni kama yameshakamilika.

Bwana Yesu ameshatupa taarifa juu ya kile kinachoitwa “chapa ya mnyama” ambayo watu watatakiwa kuwa nayo.
Imeandikwa: Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeyé aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita. (Ufunuo 13:16-18).

Utendaji wa huyu asi umejikita kwenye kudhibiti fedha; uchumi wa dunia.

Namba 666 hadi sasa iko sehemu mbalimbali – hususani kwenye sekta ileile ya pesapesa, yaani biashara na uchumi.
Kama ninavyosema kwenye makala yangu mbalimbali, lengo kuu la shetani ni kuwasomba wanadamu wengi kadiri iwezekanavyo na kuwaingiza kuzimu, na hatimaye jehanamu ya motoni ambako yeye alishahukumiwa kuwa ndiko mahali pake pa milele.

Lakini ili aweze kuwapata wengi, lengo la kwanza lilikuwa ni kuwadanganya wanadamu ili wasimwamini Mungu – kazi ambayo ameshaifanya kwa mafanikio makubwa tu. Hata hivyo, kwa vile shauku yake bado ni kubwa mno, lengo lake la pili ni kuutawala ulimwengu kwa ukaribu na uwazi zaidi kuliko alivyofanya hadi sasa. Ndio maana hivi sasa kuna ajenda ya “new world order” ambayo iko mbioni kutekelezwa.
 Mpango huu una malengo kadhaa, yakiwamo yafuatayo:
  • Kuwa na serikali moja inayotawala dunia nzima; ambayo katika ndoto ya Nebukadreza iliyofasiriwa na Danieli, ni ule ufalme wa mwisho wa vidole vya chuma kilichochanganyika na udongo(Dan. 2:33).
  • Kuwa na uchumi mmoja duniani kote.
  • Kuwa na jeshi moja la dunia nzima.
  • Kuwa na dini moja duniani kote (huenda umeshasikia juhudi mbalimbali ambazo zinafanywa sasa za kuanzisha dini hiyo, jambo ambalo linaungwa mkono na Umoja wa Mataifa). Hii ndiyo ambayo Bwana katika Ufunuo anaiita kahaba mkuu. (Ufu. 17:5).
Haya yote ni sehemu ya kutekeleza mpango wa kumleta kiongozi wa kishetani, yaani mpinga Kristo (yule asi), ambaye ataongoza dunia nzima.
Ili kuweza kudhibiti uchumi wa dunia yote pamoja na wanadamu watakaokuwapo wakati huo, inabidi uwepo mfumo wa kumfuatilia kila atakayekuwapo.

Kwa kuwa Bwana Yesu ameshatuambia kuwa hesabu ya jina la mnyama huyo ni 666, swali ni kuwa, je, kuna kitu kama hicho hivi sasa? Jibu ni ndio. Na ni mfumo ambao tunaukuta kulekule kwenye sekta ya biashara.

Mfumo huu umekuwapo duniani kwa muda mrefu sasa, huku ukiendelea kuboreshwa zaidi na zaidi kama ilivyo kwa teknolojia nyingine.

Chukua bidhaa mbalimbali – iwe ni gazeti, dawa ya meno, maji ya kunywa, mafuta ya kujipaka, sabuni ya kuogea, n.k., ukiangalia kwenye makasha au kwenye bidhaa zenyewe, utaona kitu kama hiki:
 
Hii ni kodi ya mistari (bar code). Kodi hii ina sehemu kuu mbili – sehemu ya kushoto na sehemu ya kulia. Sehemu hizo zimezungukwa na mistari mirefu zaidi ya mingine.

Namba unazoziona chini ya mchoro, upande wa kushoto, ni thamani ya mistari iliyo juu yake. Kila namba inawakilishwa na mistari miwili ya unene fulani na iliyotenganishwa na nafasi ya kiasi fulani. Mambo hayo matatu, yaani: mistari kuwa miwili, unene wa mistari na nafasi kati yake, hayabadiliki (suala la urefu halihusiki). Kwa hiyo, popote utakapoikuta mbili, mistari yake itakuwa na unene uleule na nafasi ileile kwa upande wa kushoto.
Hali kadhalika, kwa upande kulia nako namba zinakuwa na tabia hizo tatu lakini hazifanani na zile za kushoto. Tabia za kushoto ni za kushoto, na za kulia ni za kulia.
Lakini ningependa uangalie ile mistari mirefu mitatu. Ukiichunguza utaona kuwa inafanana kwa unene na nafasi kati yake. Hii inamaanisha kuwa inawakilisha namba ileile.

Sasa ili kujua hiyo ni namba gani, angalia kwenye kodi za bidhaa mbalimbali upande wa kulia (sio wa kushoto). Kisha angalia sehemu zote zenye 6. Chunguza mistari inayowakilishwa na 6. Utaona kuwa inafanana kabisa na ile iliyo mirefu. Hiyo itakuonyesha kuwa kumbe ile mistari mirefu ya katikati ni 666.

Kama nilivyodokeza hapo juu, hii ni sehemu mojawapo tu ambapo 666 inatumika.

Lakini tunachoweza kuona ni kwamba huu si mwonekano wa mwisho (final form) ya kile kitakachotumiwa na mpinga Kristo wakati wa kuitawala dunia.  

Chapa halisi ya mpinga Kristo, inadhaniwa na wengi kuwa itakuwa ni ‘electronic chip’ ndogo ambayo, kama anavyosema Bwana Yesu mwenyewe, itaweza kuwekwa kwenye mkono au usoni (hii inaonyesha kuwa ni kitu kitakachopandikizwa chini ya ngozi). Lakini bila shaka, kifaa hicho nacho kitakuwa na tabia zilezile za barcode; japo inaweza isifanane moja kwa moja na barcode za sasa.

Tabia mojawapo muhimu ya barcode ni kuwa inasomeka kielektroniki. Unapoenda kwenye supermarket, mhudumu huelekeza kwenye barcode kifaa kinachotoa namna ya mionzi fulani. Kwa sekunde moja kinasoma kila taarifa kuhusiana na bidhaa uliyochagua, kwa mfano bei yake, nk.

Lakini kwa sababu teknolojia ya chapa ya mnyama itakuwa ya juu zaidi, wale wadhibiti wa ulimwengu katika kipindi hicho, wataweza kufuatilia nyendo za kila mtu atakayekuwa amewekewa hicho kifaa.

Nihitimishe sehemu hii kwa kusema kwamba, barcodes zilizomo kwenye bidhaa madukani sasa hivi sio chapa halisi ya mpinga Kristo bali ilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya teknolojia itakayotumika (ambayo tayari ipo kazini).

Lakini kama nilivyokueleza kwenye makala yangu ya mwisho kuhusu alama za kishetani (kama hukusoma unaweza kusoma hapa), shetani amekuwa kwenye harakati zake za kumharibu mwanadamu kwa miaka na miaka. Hizi barcodes zimekuwapo kwa muda mrefu, lakini  ni sehemu kabisa ya mpango wake huo wa uharibifu – japo wengi wanaweza kuzitazama kama maendeleo ya kawaida ya kiteknolojia yaliyoletwa na mwanadamu. Kumbuka siku zote, shetani ni kerubi afunikaye. (Ezekieli 28:14).

Katika sehemu ya pili na ya mwisho ya makala haya, nitakueleza jinsi ambavyo hivi sasa teknolojia imefikia juu zaidi na tayari watu wanaanza kupandikiziwa hizo ‘chip’. Usikose sehemu hiyo.

Rafiki, usilale. Shetani anakuja; na Yesu naye anakuja! Kama wewe ni mmoja wa wale wanaosema kuwa Biblia ni uongo; au kwamba Biblia imechakachuliwa, hakuna tena muda wamalumbano na mabishano. Fungua macho yako utazame upya sawasawa! Kila kitu kiko wazi sasa!

Yafuatayo ni maneno ya Bwana wa Mbingu na nchi: Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka  mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. (Mathayo 5:18).
Kila alichokisema Mungu wa mbinguni kwenye Biblia NI LAZIMA kitimie! Na mengine ndiyo haya tunashuhudia mbele za macho yetu.

 Endelea kufuatilia pia masomo ninayoweka kwenye blog ya: www.injiliyakweli.blogspot.com na pia www.truthofgospel.blogspot.com. Ukiwa na maoni au chochote, unaweza pia kuniandikia kupitia

No comments:

Post a Comment

VANYASANGA POST TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...